Mwenye kusoma QUR'AN haozi kaburini


Ni Kweli Mwenye Kuhifadhi Qur-aan Haozi Kaburini?

SWALI:


SHUKRAN MUNGU AWAJAZI KILA LA KHERI KWA KAZI YENU. MTU AKIWA HAFIDHUL QURAN AKIFA HUWA HAOZI NAULIZA NI QURAN YOTE AMA KUHIFADHI BAADHI YA SURAH AMA JUZU FULANI ANAINGIA MTU KATIKA FADHLA HII.

FI AMANILLAH


SISTER IN ISLAM.




JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu muuliza swali. InshaAllah tutajaribu upeo wa uwezo wetu kukujibu na tawfiki inatoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala). Mwanzo tufahamu fadhila za Qur-aan ni muhimu, kubwa na nyingi, lakini ifahamike kuwa fadhila hizi zinatokana na maelezo tuyopewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na Mtume Wake, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuelezea yafuatayo katika ubora wa Qur-aan:

1.       Amesema Abu Umaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Isomeni Qur-aan kwani hakika itakuja Siku ya Qiyaama kumuombea Swahibu yake (aliyeisoma)” (Muslim).

2.       Na amesema an-Nawwaas bin Sam‘aan (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Siku ya Qiyaama italetwa Qur-aan pamoja na wale waliokuwa wakifuata maagizo yake duniani. Itamtangulia Suratul Baqarah na Aal ‘Imraan zikimtetea Swahibu yake (wale waliokuwa wakizisoma katika maisha yao)” (Muslim na at-Tirmidhiy).



3.       Na imepokewa kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mbora wenu ni yule aliyejifunza Qur-aan na akaifundisha” (al-Bukhaariy, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy).


4.       Na imepokewa kutoka kwa mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Yule ambaye anasoma Qur-aan naye ni mahiri katika hilo, atakuwa pamoja na Malaika na Mitume watukufu wenye kutii na yule ambaye anasoma Qur-aan na huku anaona ugumu na anapata shida, atapata malipo mawili” (Al-Bukhaariy, Muslim, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah).


5.       Na imepokewa kwa Abu Musa al-Ash‘ariy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mfano wa Muumini ambaye anasoma Qur-aan ni kama mfano wa mbalungi, harufu yake ni nzuri na ladha yake ni nzuri, na mfano wa Muumini ambaye hasomi Qur-aan mfano wake ni kama tende, haina harufu na ladha yake ni tamu. Na mfano wa mnafiki ambaye anasoma Qur-aan ni kama mfano wa mrehani, harufu yake ni nzuri na ladha yake ni chungu; na mfano wa mnafiki ambaye hasomi Qur-aan ni kama mfano wa handhala, hauna harufu na ladha yake ni chungu” (Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy).


6.       Na imepokewa kwa ‘Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allaah Atawanyanyua watu kwa Kitabu hichi na kuwatweza kwayo wengine” (Muslim).


7.       Na imepokewa kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna husuda isipokuwa katika mambo mawili: Mtu aliyepewa na Allaah Qur-aan, akawa anaisoma nyakati za usiku na nyakati za mchana; na mtu aliyepewa na Allaah , naye akaitoa hiyo nyakati za usiku na nyakati za mchana” (al-Bukhaariy na Muslim).



8.       Na amesema al-Baraa’ bin ‘Aazib (Radhiya Allaahu ‘anhu): Mtu mmoja alikuwa anasoma Suratul Kahf na kulikuwa na farasi aliyekuwa amefungwa karibu yake kwa kamba mbili, ukamfunika yeye ukungu (wingu) na farasi wake akawa anaogopa huku anaruka ruka na kumkimbia. Kulipopambazuka alikwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumweleza kisa hicho. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia: “Hiyo ni as-Sakiynah (utulivu) unaoteremka kwa ajili ya Qur-aan” (al-Bukhaariy, Muslim na at-Tirmidhiy).


9.       Na imepokewa kwa Ibn Mas‘uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kusoma herufi kutoka kwa Kitabu cha Allaah atapata ujira mmoja, na ujira huu ni sawa na kumi mfano wake. Wala sisemi kuwa Alif Laam Miym ni herufi moja lakini Alif ni herufi na Laam ni herufi naMiym ni herufi” (At-Tirmidhiy, na akasema niHadiyth Hasan Swahiyh na ameipokea ad-Daarimiy nayo ni Sahihi).


10.   Na imepokewa kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika yule ambaye kwamba hana moyoni mwake (yaani hakuhifadhi) chochote katika Qur-aan ni nyumba iliyohamwa” (At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh na ameipokea Ahmad, al-Haakim na ad-Daarimiy).



11.   Na imepokewa kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:“Ataitwa Swahibu (msomi) wa Qur-aan Siku ya Qiyaama na ataambiwa: ‘Soma Qur-aan na upande kuelekea (mbingu za juu) na usome kama ulivyokuwa ukisoma duniani kwani daraja yako itakuwa ni kwa ile Aayah ya mwisho utakayosoma’ (Abu Daawuud na At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadityh Hasan Swahiyh na imepokewa na Ahmad na Isnadi yake ni Hasan)”.


Hizi ni baadhi ya fadhila kutoka katika Sunnah zilizo sahihi. Bila shaka zipo fadhila za kusoma Aayah na surah Fulani zilizomo katika Qur-aan. Hata hivyo, wapo watu ambao wamebuni Hadiyth ili kuonyesha utukufu ambao haumo kabisa katika Qur-aan. Mfano ni ile inayosemekana ni Hadiyth lakini ni ya kubuni: “Msomaji wa Qur-aan hawi mzulufu”.

Ama fadhila hii kwa mwenye kuhifadhi Qur-aan kuwa hataoza haijapatikana katika Hadiyth zilizo sahihi. Hakika wale ambao miili haitaoza kwa Hadiyth sahihi ni Mitume. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
yao
Allaah Aliyetukuka, Ameiharamisha ardhi kula miili ya Mitume” (Muslim, Abu Daawuud, an-Nasaaiy na Ibn Maajah kutoka kwa Aws bin Aws [Radhiya Allaahu ‘anhu]).


Na katika Hadiyth nyingine Abu Dardaa’ (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Niswalieni Ijumaa kwani kufanya hivyo kunashuhudiwa. Malaika wapo kwayo, na hakuna atakayeniswalia bila Swalah yake hiyo kuletwa kwangu mpaka anakaposimama. Nikamuuliza: ‘Je, hayo pia yatakuwa baada ya kuaga dunia kwako?’ Akasema: ‘Allaah Ameiharamisha ardhi kuila miili ya Manabii’. Hivyo, Mtume wa Allaah yu hai (uhai wa maisha ya Barzakh) na anaruzukiwa” (at-Tirmidhiy na Ibn Maajah).

sana
Kuhifadhi Qur-aan kuna fadhila zake lakini pamoja na kufuata maagizo yaliyomo ndani yake na kukatazika na maharamisho. Kuhifadhi bila kufuata inakuwa haina fadhila kwani Qur-aan yenyewe itakuwa inakulaani nawe huna hata habari kwa yale matendo unayoyafanya.

Na Allaah Anajua zaidi.